Wajibu wa Mwanadamu

Watu wengi hutafuta umaarufu, heshima, mamlaka na mali bila kujua au wakiwa wamesahau maana na kusudi la kweli la maisha. Hufanya kazi kwa bidii na kujikusanyia maarifa mengi ili waishi kwa wingi na kutimiza malengo yao. Wanapotimiza malengo hayo, huenda wakaonekana wamefanikiwa kwa muda, lakini mwisho wa taabu na jasho lao chini ya jua ni nini?

Kila walichofanya kitakuwa bure miili yao itakaporudi kuwa konzi ya mavumbi; kisha hukumu na adhabu ya milele itawangoja. Sulemani, mfalme wa Israeli, alikuwa na utajiri, heshima, umaarufu na mamlaka makubwa kuliko mtu mwingine yeyote. Lakini mwishoni mwa maisha yake alikiri, “Ubatili mtupu, ubatili mtupu; yote ni ubatili.”

Mwanadamu ana faida gani katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua? Nimeyaona matendo yote yaliyotendeka chini ya jua; tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo. Kisha mfalme anatuhimiza, “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.” Kila jambo ambalo mtu amefanya chini ya jua litatoweka anapokufa, kwa hiyo yote ni bure.

Hata hivyo, ukimkumbuka Mungu Muumba wako na kupata uzima wa milele, utaishi katika utukufu na heshima katika Ufalme wa Mbinguni milele. Huo si ubatili hata kidogo. Ndiyo maana mtu mwenye hekima hujitahidi kuishi kwa furaha mbinguni milele. Tufanye nini ili tupate uzima wa milele? Zaidi ya yote, tunapaswa kutimiza wajibu wa mwanadamu ambao Mungu Muumba ametuamuru. Mhubiri 12:13 inasema, “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; mche Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.”

Ili kupata uzima wa milele, unapaswa kutambua kwamba matendo yote uliyoyafanya kwa ajili ya tamaa zako za dhambi ni bure na kuyaacha; unapaswa kumpenda Mungu, kuzishika na kuzitii amri zake. Kwa kusudi hilo, mpokee Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wako. Alisulubiwa na kufufuka ili kuwakomboa wanadamu wote kutoka katika dhambi zao. Kisha, kwa Neno la Mungu, chunguza na uondoe dhambi na uovu wako moja baada ya nyingine, ili uweze kushinda majaribu na magumu ya kila aina kwa imani isiyotikisika na kuishi kwa utukufu wa Mungu katika kila jambo unalofanya, iwe unakula au unakunywa.

Ninaomba kila mmoja wenu atambue kwamba kumcha Mungu na kuzitii amri zake ndiko kutimiza wajibu wa mwanadamu na kupata uzima wa milele; na ndiko kunakowezesha kufurahia mapendeleo na baraka anazopewa mtoto wa Mungu. Ishi maisha yenye baraka za kweli. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life